Maswa. Wananchi wa Kata ya Masela, wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wanalazimika kusafiri zaidi ya kilomita 50 kufuata huduma za polisi, hali inayowaongezea gharama za usafiri na kuwapa changamoto wanapohitaji kuripoti matukio ya uhalifu.
Wamesema umbali huo pamoja na muda wanaotumia kufika kituoni unaweza kuchelewesha utoaji wa taarifa za uhalifu na upatikanaji wa msaada wa haraka, hasa pale matukio yanapohitaji hatua za haraka za kiusalama.
Changamoto hiyo inatokana na kata hiyo kuwa mpakani mwa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu na Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, hali inayofanya wananchi kuona umuhimu wa kusogeza huduma za polisi karibu na makazi yao.
Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Oktoba 22, 2026, wakazi hao wameiomba Serikali kuanzisha kituo cha polisi katika kata hiyo ili kurahisisha utoaji wa taarifa za uhalifu na upatikanaji wa huduma za kiusalama.
Mapambano Jackson, mkazi wa kijiji cha Masela wilaya ya Maswa akitoa maoni yake juu ya uanzishwaji wa kituo cha polisi katika eneo hilo. Picha na Samwel Mwanga
Mapambano Jackson, mkazi wa eneo hilo, amesema umbali wa kufuata huduma za polisi ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi ili kuwawezesha wananchi kuripoti matukio kwa wakati.
“Tunapotaka kuripoti tukio, tunalazimika kusafiri zaidi ya kilomita 50 kufika kituo cha polisi. Wakati mwingine tukio linakuwa limepita au ushahidi unapotea kwa sababu ya kuchelewa kufika,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Masela wakiwa kwenye mkutano wa kujadili hali ya usalama katika kijiji hicho.Picha na Samwel Mwanga
Mkazi mwingine, Raphael Muchael, amesema gharama za usafiri ni kubwa kutokana na umbali wa kituo cha polisi, hali inayowafanya baadhi ya wananchi kushindwa kuripoti matukio kwa wakati.
Kwa upande wake, Suzana Jinasa amesema, “Tuna matumaini kituo hicho kikianzishwa kitasaidia kupunguza umbali na gharama za usafiri. Pia wananchi wataweza kupata msaada wa polisi kwa wakati na kujisikia salama zaidi,” amesema.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, .Picha na Samwel Mwanga
Akizungumzia ombi hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amesema Jeshi la Polisi lina mpango wa kuanzisha kituo cha polisi katika Kata ya Masela ili kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiusalama kwa wakazi ambao kwa sasa hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Katika kuunga mkono mpango huo, Chifu Antonia Sangalali, mkazi wa eneo hilo, amejitolea nyumba yake kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho.



Leave a Reply