Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) unaanzisha mpango mpya wa kushughulikia matumizi ya akili mnemba (AI) katika shughuli za kijeshi, ukiwa na lengo la kukabiliana na wasiwasi kuhusu hatari ambazo teknolojia hiyo inayokua kwa kasi inaweza kusababisha kwa binadamu.
Mpango huo unakuja wakati UN ikiadhimisha miaka 81 tangu kuanzishwa kwake Oktoba 24, 1945, ikiwa ni taasisi inayoyaleta pamoja mataifa yote ulimwenguni kwa lengo la kuzuia migogoro baina yao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, mpango huo unaoandaliwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Kupunguza Silaha (UNIDIR), unatarajiwa kuanzisha jukwaa la kwanza la kimataifa litakalowakutanisha wadau muhimu kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Mkuu wa taasisi hiyo yenye makao yake Geneva, Robin Geiss ameonya katika mkutano na waandishi wa habari wa UN uliofanyika juzi kwamba, “nafasi ya binadamu kufanya uamuzi inazidi kuwa finyu, ikiwemo katika masuala yanayohusu silaha za nyuklia.”
Geiss amesema ni vigumu kutathmini dunia imekaribia kwa kiasi gani kufikia hatua ambayo mashine zinaweza kuchukua hatua nje ya udhibiti wa binadamu. Alisema kutokuwa na uhakika kuhusu suala hilo ndiko kunakolengwa kutatuliwa kupitia mpango huo.
Ameeleza kuwa changamoto mojawapo ni kuongezeka kwa matumizi ya AI katika maeneo mengi, yakiwemo mifumo ya tahadhari za mapema, ukusanyaji wa taarifa na upelelezi.
Amesema hali hiyo inafanya iwe vigumu kubaini ni wakati gani hasa binadamu wanaweza kuanza kupoteza udhibiti wa teknolojia hiyo.
Kwa mujibu wa Geiss, kwa muda mrefu kumekuwa na kusitasita kwa kiwango kikubwa kuhusu kuweka mifumo ya udhibiti na ulinzi wa matumizi ya AI.
Hata hivyo, kuenea kwa uwezo wa teknolojia hiyo na athari zinazoweza kutokea kutokana na matumizi yake kumechangia kuongezeka kwa uelewa kwamba dunia imefikia wakati muhimu wa kuchukua hatua, ikiwemo katika matumizi ya AI kijeshi.
Geiss amesema UN inatambua kuwa ushindani wa kimataifa wa kuongoza katika teknolojia ya AI ni kikwazo kikubwa katika juhudi za kuweka udhibiti wake.
“Hata hivyo, wasiwasi kuhusu athari za AI tayari umevuka mipaka ya makundi ya kisiasa na kijiografia, na unachochea hatua kutoka kwa mataifa makubwa,” amesema.
Ametoa mfano wa pendekezo lililotolewa mwezi uliopita la Marekani na China kuanzisha mfumo wa tahadhari kuhusu usalama wa AI, kwa ajili ya kushughulikia masuala yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Hatari zinazotokana na matumizi ya AI pia zilikuwa miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa katika hotuba za viongozi wa nchi nyingi kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wao wa ngazi ya juu uliofanyika mwezi uliopita.
Wakati UN ikigeukia mpango huo, Serikali ya Tanzania itashirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 81 ya Umoja wa Mataifa katika Kujenga Mustakabali wa Amani, Utu na Uendelevu kwa Wote.”
Siku ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa Oktoba 24 ya kila mwaka kutafakari mafanikio ya Umoja huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945 na kuimarisha dhamira ya kimataifa ya kukuza amani, ushirikiano na maendeleo endelevu.
Tangu Tanzania ijiunge na Umoja wa Mataifa mwaka 1961, imekuwa ikishirikiana na umoja huo kulinda amani na usalama, kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kukabiliana na changamoto za kibinadamu na kimazingira.
Ushirikiano huu unaongozwa na Mfumo wa Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa kwa Maendeleo Endelevu nchini Tanzania (2022-2027), unaounga mkono vipaumbele vya kitaifa na utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Tanzania na Umoja wa Mataifa zinaendelea kuhimiza hatua za pamoja za kuimarisha ustahimilivu, kupanua fursa na kuhakikisha maendeleo jumuishi, hususan kwa vijana kuelekea mwaka 2030.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa Tanzania inawaalika washirika na jamii kushiriki katika kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa, pamoja na kutafakari wajibu wa pamoja wa kujenga mustakabali unaozingatia amani, heshima na uendelevu kwa wote.


Leave a Reply