Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mgandamizo mdogo wa hewa uliopo katika Bahari ya Hindi karibu na Visiwa vya Ushelisheli unatarajiwa kuimarika na kuwa kimbunga ndani ya siku nne zijazo.
Pia, ukitarajiwa kuimarisha mifumo ya mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani kuanzia Oktoba 24, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA jana, Jumanne, Oktoba 20, 2026, mgandamizo huo upo umbali wa takribani kilomita 1,600 kutoka pwani ya Tanzania na unaelekea katika ukanda huo.
Taarifa hiyo imeeleza uwepo wa mfumo huo katika Bahari ya Hindi unatarajiwa kuimarisha kwa kiasi mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya pwani ya Tanzania na maeneo jirani, hususan kuanzia Oktoba 24, 2026.
Hata hivyo, TMA haijataja maeneo mahususi yatakayopata mvua hizo wala kiwango cha mvua kinachotarajiwa katika kila eneo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imewataka watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri pamoja na miongozo ya wataalamu wa sekta husika.
TMA imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo wa hewa na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini, na itaendelea kutoa taarifa kwa umma kadiri itakavyohitajika.


