Shinyanga. Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amekamatwa usiku akiwa nyumbani kwake, akashikiliwa kwa saa kadhaa na baadaye kuachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga.
Obadi anadaiwa kupanga maandamano yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2026.
Kigogo huyo wa Chadema alikamatwa saa 8 usiku wa leo Jumatano, Oktoba 21, 2026 na kuachiwa leoleo saa 5 asubuhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kukamatwa na kuachiwa kwa kiongozi huyo, ingawa hakueleza sababu za kina za kushikiliwa kwake.
“Alikamatwa jana na tayari ameachiwa kwa dhamana, asante,” amesema Magomi.
Akisimulia tukio hilo Jumatano, Oktoba 21, 2026, muda mfupi baada ya kuachiwa, Obadi alisema hakutarajia kukamatwa, hivyo alishtuka kusikia hodi mlangoni katikati ya usiku.
“Baada ya kusikia hodi, ilinilazimu kuchungulia dirishani ndipo nilipowaona askari. Ikabidi nijipe muda na familia ili kutafakari zaidi. Wakati nikitafakari, waliendelea kugonga kwa muda mrefu kabla ya kuondoka na baadaye kurudi tena,” amesema.
Amesema wakati akitafakari hatua ya kuchukua, askari hao waliondoka, lakini baadaye walirejea wakiwa wameambatana na mwenyekiti wa serikali ya mtaa anakoishi, aliyemshawishi afungue mlango.
“Walivyorudi, walikuwa na mwenyekiti wangu wa serikali ya mtaa, ambaye akaniambia nifungue kwa sababu amani imetawala,” ameeleza Obadi.
Hata hivyo, alisema hakuridhika mara moja na maelezo hayo, akihofia kufungua mlango wakati huo wa usiku bila kufahamu kilichokuwa kikiendelea.
Amesema alimuuliza tena mwenyekiti huyo sababu za kufika nyumbani kwake muda huo kabla ya kuamua kufungua mlango baada ya kuhakikishiwa kuwa amani imetawala.
Obadi alisema baada ya kufungua mlango, aliwakuta askari sita, watatu kati yao aliwafahamu wakiwa karibu naye, huku wengine watatu wakiwa kwenye gari.
Amesema aliambatana na askari hao hadi Kituo cha Polisi Kahama, ambako alianza kutoa maelezo kuhusu tukio hilo.
“Nilipofika kituoni nilitoa maelezo ya awali, lakini sikuendelea sana kwa sababu sikuwa na wakili wangu wakati huo. Hivyo, nikawaomba maelezo mengine niyatoe nikiwa na mwanasheria,” alisema.
Amesema baada ya kueleza msimamo huo, aliwekwa rumande, ingawa alielezwa kuwa dhamana ilikuwa wazi na angeweza kuachiwa baada ya kutimiza masharti yaliyotakiwa na Polisi.
“Tuhuma walizonieleza ni kupanga maandamano ya Oktoba 29, 2026,” alisema Obadi.
Aliongeza kuwa baada ya kuachiwa kwa dhamana, alitakiwa kurejea kituoni hapo Alhamisi asubuhi kwa ajili ya hatua nyingine za uchunguzi.
Awali, kabla ya Obadi kuachiwa, wakili wake, Alex Masaba, aliliambia Mwananchi kuwa kiongozi huyo alikuwa akishikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kupanga maandamano yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2026.
Kwa mujibu wa Masaba, baada ya kuchukuliwa maelezo yake, Obadi alielezwa kuwa dhamana ilikuwa wazi, huku akitakiwa kuwa na mdhamini mmoja ili aweze kuachiwa.
Kiongozi mwingine ashikiliwa
Kukamatwa na kuachiwa kwa dhamana kwa Obadi kunatokea wakati kukiwa na tukio jingine la kiongozi wa Chadema kushikiliwa na Polisi, siku nane baada ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Mafunzo, Oganaizesheni na Uchaguzi wa chama hicho, John Pambalu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa awali, Pambalu alikuwa akiendelea na mahojiano na Polisi jijini Dar es Salaam.
Kukamatwa kwa viongozi hao kumeibua maswali kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya viongozi wa chama hicho katika kipindi kinachotangulia tarehe inayotajwa ya maandamano.
Hata hivyo, hadi sasa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga halijaeleza kwa kina sababu za kumshikilia Obadi, zaidi ya kuthibitisha kukamatwa na kuachiwa kwake kwa dhamana.



Leave a Reply