Rais Mwinyi arejea Zanzibar, ataja matokeo chanya ziara ya siku 10 ughaibuni

Rais Mwinyi arejea Zanzibar, ataja matokeo chanya ziara ya siku 10 ughaibuni

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amerejea nchini baada ya kukamilisha ziara zake za kiserikali katika nchi za Qatar, Armenia na Hispania huku akitaja mafanikio ya ziara hizo.

Amesema ziara hizo zililenga kufungua fursa za kuimarisha uwekezaji, kushiriki mijadala ya kimataifa kuhusu hifadhi ya mazingira na kuimarisha maendeleo ya michezo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya kurejea nchini jioni ya leo Jumapili, Oktoba 18, 2016, Dk Mwinyi ameeleza mazungumzo na mikutano aliyoshiriki itakuwa na matokeo chanya kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Nchini Qatar, ziara ya Rais Mwinyi ilipata mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji na biashara.

“Nilikutana na wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali walioonesha nia thabiti ya kuwekeza Zanzibar, hususan katika sekta za hoteli na ujenzi wa nyumba za makazi,” amesema.

Miongoni mwa kampuni kubwa alizokutana nazo ni Al Alfardan inayojihusisha na ujenzi wa hoteli na makazi, ambayo imeahidi kuja Zanzibar kutathmini na kuendeleza fursa za uwekezaji hasa katika maeneo ya mashariki ya Unguja.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuvutia watalii wengi zaidi kutoka ukanda wa Mashariki ya Kati, kuongeza upatikanaji wa nyumba za makazi na kufungua fursa nyingi za ajira kwa wananchi.

Ili kuweka mazingira rafiki na yanayozingatia sheria, amesema Serikali imeunda timu maalumu kwa ajili ya kuchunguza masuala yanayoathiri biashara zitakazobainisha hatua za kuchukuliwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Uhifadhi wa mazingira na bayoanuwai Akiwa nchini Armenia, Dk Mwinyi alimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika mkutano wa kimataifa uliolenga masuala ya uhifadhi wa mazingira na baioanuwai.

Amesema majadiliano katika mkutano huo yalilenga ushirikiano wa kimataifa wa kudhibiti uharibifu wa mazingira na utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia juhudi za uhifadhi zinazozingatia mahitaji ya jamii.

Rais Mwinyi alibainisha changamoto kuu za kimazingira zinazoikabili Zanzibar, ikiwemo mmomonyoko wa fukwe, kuingiliana kwa maji ya chumvi kwenye visima vya maji safi na kukauka kwa visima.

“Juhudi za kulinda rasilimali za bahari na nchi kavu zinapaswa kuzingatia pia vyanzo vya kipato na vyakula kwa wananchi wanaotegemea rasilimali hizo,” amesema huku akiahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa masuala yote yaliyojadiliwa.

Sekta ya michezo ilipata mafanikio makubwa kupitia ziara kwa mujibu ya Dk Mwinyi mjini Madrid, Hispania.

Amesema akiwa nchini humo, alitembelea klabu maarufu ya Real Madrid na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Real Madrid Foundation na kampuni ya Unicorn Sports Zanzibar Limited.

Amesema ushirikiano huu unalenga kukuza na kuibua vipaji vya soka kwa vijana wa Zanzibar kupitia hatua mbalimbali.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Real Madrid Foundation itatoa makocha watakaokuja Zanzibar kutoa mafunzo kwa vijana na kuwajengea uwezo makocha wa ndani ili waweze kubaini, kulea, na kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi.

“Katika kipindi cha wiki mbili hadi tatu zijazo, utaratibu wa kutembelea na kukagua viwanja vya michezo utaanza, sambamba na kuandaa kliniki za soka,” amesema.

Viwanja vilivyotajwa kusaidia programu hizi ni pamoja na Amaan, Mao na Fumba.

Amesema mpango huo unalenga kuanzisha Akademi ya Real Madrid Zanzibar itakayotoa mafunzo rasmi kwa utaratibu maalumu na kuimarisha uwezo wa vijana kushindana katika viwango vya juu.

“Ushirikiano huu utawapa vijana waliotayari fursa ya kupata nafasi za kucheza katika klabu za nje ya nchi pale watakapofikia viwango vinavyohitajika,” amesema.

Dk Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha miundombinu ya michezo ili kuhakikisha vijana wanatumia vipaji vyao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Source link