Bunda. Nyumba zaidi ya 360 zimepata madhara mbalimbali ikiwepo kubomoka kufuatia mvua zilizoambatana na upepo mkali kunyesha katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya familia zimelazimika kupata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki huku Serikali ikitoa msaada wa chakula kwa familia hizo.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jumamosi Oktoba 24, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Halfan Haule alipozungumza na Mwananchi ambapo amesema tathmini ya athari ya mvua hizo inaendelea.
Amesema kati ya nyumba hizo, nyumba 50 zimebomoka kabisa na hazifai kwa matumizi tena na kwamba hadi sasa kata tatu wilayani humo ndizo zilizoathiriwa na mvua hizo.
Ameeleza kuwa mvua hizo zilinyesha Oktoba 21 na 22, mwaka huu, ambapo kata zilizoathirika ni Kabasa, Hunyari na Mcharo zote za halmashauri ya Mji wa Bunda.
“Katika Mtaa wa Nyamilama, nyumba 65 zimeathirika na nyumba sita kati ya hizo zimeanguka kabisa na chakula kimesombwa na maji, familia zimehifadhiwa kwa ndugu, tumepita katika maeneo yote na mahitaji ya kwanza tumeona ni chakula hivyo tumetoa chakula kwa waathirika,” amesema.
Ametoa wito kwa wadau kuchangia vifaa vya ujenzi ili kuwezesha wamiliki wa nyumba hizo kurejesha makazi yao katika hali ya kawaida na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Pia, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho kwa nyumba zenye changamoto ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Diwani wa Kabasa, Daniel Magembe amesema katika kata yake zaidi ya nyumba 135 zimeathirika huku nyumba 11 zikibomoka kabisa na kusababisha kaya hizo kukosa chakula kutokana na vyakula kuharibika baada ya nyumba kubomoka.
Amesema hali hiyo inesababisha pia wamiliki wa nyumba hizo kupoteza mali zao kwani hawakuweza kuokoa kitu chochote.
“Kaya hizo hivi sasa zimepata hifadhi kwa ndugu, tunashukuru Serikali imefika na kuona hali ilivyo ambapo pia waathirika wamepata msaada wa vyakula,” amesema.
Akiwa kwenye kikao na viongozi wa dini mjini Musoma, jana, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi aliwataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua za El- Nino.
Amesema tayari mvua hizo zimeanza kunyesha na madhara kadhaa kutokea ambapo alisema mbali na nyumba kuathirika pia mvua hizo zilisomba daraja moja wilayani Bunda na kwamba tayari daraja hilo limetengenezwa na huduma zimerejea kama kawaida.
“Kwa mkoa wetu madhara yametokea katika wilaya za Bunda na Rorya lakini hakuna madhara kwa binadamu niwaombe viongozi wa dini kupitia nyumba za ibada endeleeni kuwahamasisha wananchi wachukue hatua ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika,” alisema.
Alisema wakati watu wakichukua tahadhari wananchi wanatakiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi kwa maelezo kuwa suala la El- Nino lisiwe kikwazo cha kuendelea na shughuli hizo.


Leave a Reply