“Tofauti na zamani, sasa hivi nina sehemu nyingi za kutunza fedha zangu na zikawa salama. Kuna benki, kuna simu, kuna bondi, saccos, UTT na nyinginezo na si tu kuhifadhi hata kuwekeza kwa namna inayonipa faida. Hata kama ni pesa ya jumuiya bado inaweza kuwekwa sehemu mbalimbali na ikawa salama,” anasema Eliudi Allen Mkazi wa Dar es Salaam.
Uozefu wa Allen pengine unafanana na wa wengi katika zama hizi ambazo pamoja na kuimarika kwa sekta ya benki, simu nayo imekuwa benki ya mkononi, kibubu cha kidijitali, pochi ya kidijitali na dirisha na mikopo lisilo na mlolongo mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa FSDT ya Machi, 2025 Huduma za fedha kwa njia ya simu ndizo zinazoongoza katika kukuza ujumuishi rasmi wa kifedha nchini Tanzania, huku matumizi yake yakifikia asilimia 72 ya wananchi, kiwango kinachozidi kwa mbali huduma za kawaida za benki za biashara, ambazo zinafikia asilimia 22.
Aidha, Ripoti ya robo ya pili ya mwaka 2026 iliyoishia Juni, 2026 inaonyesha kuwa akaunti hai za miamala ya simu ziliongezeka na kufikia watumiaji hai milioni 87.04 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya akaunti milioni 10 kutoka milioni 75.78.
Ripoti hiyohiyo, inaonyesha miamala ya simu inayofanyika kwa mwezi imefikia milioni 710.9 ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 21 ilikinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025. Katika miaka ya hivi karibu huduma za miamala ya simu zimeunganishwa na mfumo wa malipo ya haraka (TIPS) na TANQR hivyo kuongeza mvuto kwa watumiaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu Tanzania (BoT) kuhusu mifumo ya malipo kwa mwaka 2025, miamala iliyofanyika kwa njia ya simu katika mwaka husika ilifikia Sh255.13 ikiwa ni ongezeko la asilimia 28.30 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa idadi ya miamala ya kuweka akiba kidijitali iliongezeka mara dufu mwaka 2025, kwa ukuaji wa asilimia 110 hadi kufikia miamala milioni 97.53. Thamani ya jumla ya fedha zilizowekwa kama akiba kidijitali iliongezeka kwa asilimia 263 hadi kufikia Sh3.18 trilioni, kutoka Sh1.21 trilioni mwaka 2024.
Kwa upande wa mikopo ya kidijitali miamala milioni 336.52, yenye thamani ya Sh5.58 trilioni mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32.29 la thamani ya mikopo hiyo ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Katika moja ya mkutano wa kutangaza kwa kiwango cha riba ya Benki Kuu (CBR) mmoja wa viongozi wa benki alikiambia chombo hicho cha juu cha usimamizi wa fedha (BoT) kuwa kuna haja ya kuangalia hali ya kuibuka kwa taasisi nyingi za uwekezaji katika soko la fedha jambo ambalo alisema linaweza kusababisha benki hizo kukosa amana za kutosha.
Pamoja na hoja hiyo, BoT ililitazama jambo hilo kama ukuaji wa soko na kupanuka kwa fursa za uwekezaji na huduma za kifedha nchini. Katika ripoti yake ya mifumo ya malipo kwa mwaka 2025 ilieleza kuwa huduma za fedha kidijitali zimeendelea kuimarisha soko la fedha huku matumizi ya cheki yakizidi kupungua.
Hata hivyo Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) unasema huduma mpya zilizoibuliwa na mapinduzi ya kiteknolojia hazijameza biashara ya benki badala yake, imebadilisha mfumo wa utoaji huduma, kupunguza gharama za miamala na kufungua fursa mpya za biashara.
“Teknolojia haijachukua nafasi ya benki, imebadilisha namna benki zinavyofanya biashara na kuwafikia wateja wake kulinga na mahitaji yao. Benki zitakazofanikiwa ni zile zitakazotumia teknolojia kuongeza thamani kwa wateja,” anasema Theobald Sabi ambaye ni Mwenyekiti wa TBA.
Anasema ni kweli kuna ukuaji wa huduma za kifedha kupitia simu umebadilisha kwa kiasi kikubwa namna Watanzania wanavyotumia huduma za benki hivyo badala ya kuangalia teknolojia kama tishio, benki zinaendelea kuitumia kama nyenzo ya kuongeza ufanisi, kuboresha uzoefu wa wateja, kupanua wigo wa huduma na kukuza biashara.
Anasema kutokana na kupanuka kwa soko la fedha na njia mbadala za kupata huduma hivi sasa, wateja wanatarajia kupata huduma za malipo, akiba, mikopo na bima kwa haraka, kwa usalama na wakati wowote bila kulazimika kufika katika matawi ya benki.
Anasema kutokana na kupanuka kwa soko la fedha na njia mbadala za kupata huduma hivi sasa, wateja wanatarajia kupata huduma za malipo, akiba, mikopo na bima kwa haraka, kwa usalama na wakati wowote bila kulazimika kufika katika matawi ya benki.
Sabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Banki ya NBC anasema pamoja na maendeleo haya, benki zinaendelea kuwa na jukumu muhimu katika ukusanyaji wa amana, utoaji wa mikopo, usimamizi wa vihatarishi, ulinzi wa fedha za wateja na ufadhili wa biashara na miradi mikubwa ya maendeleo.
“Kwa upande wa NBC, tunaendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali kupitia NBC Kiganjani na NBC Connect, sambamba na kupanua mtandao wa mawakala na matawi kwa lengo la kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa urahisi, usalama na kwa namna inayokidhi mahitaji yao yanayobadilika”.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya FinScope Tanzania, matumizi ya huduma za benki miongoni mwa watu wazima yaliongezeka kutoka asilimia 16.7 mwaka 2017 hadi asilimia 22.2 mwaka 2023. Katika kipindi hicho, ujumuishaji wa kifedha kupitia huduma rasmi uliongezeka kutoka asilimia 65 hadi 76.
Aidha, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania, zinaonyesha kuwa idadi ya mawakala wa benki ilifikia 189,719 Desemba 2025, kutoka 59,291 Juni 2022. Ukuaji huu unaonesha namna benki zinavyopanua huduma nje ya matawi ya kawaida na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wa watoa huduma za kifedha kwa njia ya simu wanasema mustakabali wa huduma za kifedha hautakuwa wa benki pekee wala kampuni za mawasiliano pekee bali utakuwa mfumo unaounganisha benki, kampuni za mawasiliano, watoa huduma za fedha za kidijitali, wafanyabiashara na watoa huduma wengine wa teknolojia.
Mkuu wa fedha na malipo ya kidijitali wa kampuni ya Mixx by Yas Mshamma Mshamma anasema benki zitaendelea kuwa na nafasi muhimu katika mfumo wa kifedha, hasa katika usimamizi wa fedha, ufadhili, uwekezaji na huduma na kampuni za mawasiliano zina uwezo wa kufikisha huduma hizi kwa watu wengi kupitia teknolojia, mtandao wa mawakala wake.
“Kwetu sisi ushirikiano na benki ni sehemu muhimu ya namna tunavyopanua huduma zetu. Kwa mfano, bidhaa zetu za mikopo na akiba zinategemea ushirikiano na taasisi za kifedha katika maeneo mbalimbali. Ushirikiano huu unatupa fursa ya kuunganisha teknolojia inayomfikia mteja na uwezo wa kifedha na utaalamu wa washirika wetu,” anasema.
Mshamma anasema kwa kiasi kikubwa, huduma za fedha kwa njia ya simu zimebadilisha namna Watanzania wanavyopata, wanavyotumia na kusimamia fedha zao na mabadiliko makubwa yanayoonekana ni kwamba huduma za kifedha zimekuwa karibu zaidi na maisha ya kila siku ya watu.
“Mfano sisi Mixx mbali na huduma tunazozitoa sasa tunaendelea kujenga mfumo unaounganisha malipo, mikopo, akiba, bima na uwekezaji. Lengo letu si kuwezesha watu kutuma na kupokea fedha pekee, bali kuwasaidia kutumia fedha zao kwa ufanisi zaidi na kupata fursa pana za kiuchumi,” anasema.
Alitolea mfano huduma yao ya kibubu inawapa wateja njia ya kuweka akiba kidijitali muda wowote, na kibubu plus inawapa wateja njia ya kuweka akiba kidijitali kwa muda maalumu wakati Kikoba kinasaidia vikundi kusimamia akiba zao kwa kutumia teknolojia.
Kuhusu usalama wa huduma za fedha kwa kampuni za kidijitali Mshamma anasema mafanikio ya huduma hizi hayapimwi kwa idadi ya mikopo inayotolewa pekee, bali pia kwa uwezo wa wateja kutumia huduma hizo kwa usalama na kuendelea kunufaika nazo.
“Tunataka simu ya mteja iwe lango la kupata huduma mbalimbali za kifedha, kuanzia malipo na mikopo hadi akiba, bima na uwekezaji ila ni muhimu kuelewa kwamba ukuaji wa huduma za kifedha za kidijitali unapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa wateja, uwazi na matumizi yenye uwajibikaji,” anasema Mshamma.
kuhusu mabadiliko hayo ya soko fedha Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai anasema mabadiliko yanayoonekana yanatokana na teknolojia kuleta suluhisho nyingi rahisi na watu wanafurahia kuzitumia lakini haimaanishi kuwa zina athiri hasi katika biashara ya huduma za kifedha.
“Ni kweli sasa kuna malipo kidijitali, mikopo kidijitali, bima na uwekezaji kupitia simu lakini wote hao pesa zao zinalala benki kwakuwa hawana mifumo ya kibenki, hata fedha zinazozunguka katika simu zinakuwa zimetokea benki na zitakwenda benki,” anasema.
Anasema mabadiliko yanayoshuhudiwa hivi sasa ni neema kwa watumiaji kwani sasa mawanda ya huduma yamerahisishwa hivyo machaguo ni mengi jambo linalofanya watoa huduma kuongeza na kuboresha huduma zao.
“Benki hazijaathirika isipokuwa ni fursa nzuri kwa wateja kuchagua zaidi kile wanachoona kinawapa faida. Majukwaa mapya ya huduma yameanzishwa na yanahudumia watu wengi lakini benki nyingi bado zinapata faida kubwa hivyo hazijatikishwa,” anasema mtaalamu huyo wa masuala ya fedha.
Hata hivyo anasema soko litaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa akiitaja teknolojia ya Akili Unde kama jambo ambalo nalo linaanza kuchangamsha soko, hata hivyo Dk Swai alisisitiza kuwa ushindani huo ni mzuri.
Dk Swai alisisitiza kuwa pamoja na mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa bado kuna watu wanaamini katika mifumo ya jadi ya huduma za kifedha na kwa sababu masuala ya fedha yanategemea zaidi imani, hivyo wao hawajihusishi na mambo mapya yanayotokea.



Leave a Reply