Marekani kufungua milango kwa startups za Tanzania

Marekani kufungua milango kwa startups za Tanzania

Marekani kufungua milango kwa startups za Tanzania

Dar es Salaam. Marekani iko tayari kushirikiana na kampuni bunifu za Tanzania zinazobuni bidhaa na huduma za kiteknolojia, huku mitaji, ubia na upatikanaji wa masoko vikitajwa kuwa muhimu katika kukuza biashara hizo na kuziimarisha katika ushindani wa kimataifa.

Balozi wa Marekani nchini, William Trachman, amesema wajasiriamali wanapaswa kuunganisha mawazo yao na mifumo endelevu ya biashara, huku wakijenga uhusiano na wawekezaji na kampuni zinazoweza kuwasaidia kupanua shughuli zao.

Akizungumza leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, katika wiki ya maonyesho ya biashara bunifu 2026 yanayofanyika kwa siku tano jijini Dar es Salaam, Trachman amesema anatarajia kuona vijana wa Tanzania wakishirikiana na kampuni za Marekani katika kukuza teknolojia na biashara zao.

Amesema Tanzania ina fursa kutokana na uwezo na ari ya vijana wake, lakini mafanikio yanahitaji juhudi, ubunifu na utayari wa kufanya maamuzi magumu ya kibiashara.

“Ningependa kuona baadhi ya kampuni hizi zikifanya kazi na kampuni za Marekani katika siku za karibu,” amesema.

Balozi huyo amewataka wajasiriamali kujenga mitandao ya uhusiano wa muda mrefu, akieleza kuwa kushirikiana na wawekezaji, wafanyabiashara na wabunifu wengine kunaweza kufungua milango ya maendeleo ya biashara.

Ametolea mfano Silicon Valley, kitovu cha teknolojia nchini Marekani, akisema mafanikio ya kampuni nyingi yamechangiwa na kubadilishana mawazo na ushirikiano kati ya waanzilishi wa biashara.

Amesisitiza kuwa kampuni changa zinapaswa kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji halisi ya watu na kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia badala ya kutegemea bidhaa zilizopo pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani unaweza kuziwezesha kampuni changa kupata uwekezaji, teknolojia na masoko mapya.

Ameitaja Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA) kuwa miongoni mwa fursa ambazo wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza kutumia kupanua mauzo yao nchini Marekani, kwa kuzingatia masharti ya mpango huo.

AGOA hutoa upendeleo wa ushuru kwa bidhaa zinazostahili kutoka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinazokidhi vigezo vilivyowekwa na Marekani.

“Ni fursa nzuri kwa vijana wa Tanzania ambao wana ndoto za kuuza katika soko kubwa kama Marekani,” amesema Muhaji.

Amesema TSA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Marekani kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kuhakikisha kampuni changa zinapata fursa za kukuza biashara zao.

Hata hivyo, amesema kampuni zinazolenga soko hilo zinapaswa kuelewa masharti yanayohusu bidhaa, viwango vya ubora na taratibu za kuingiza bidhaa nchini Marekani.

Mjumbe mwanzilishi wa bodi ya TSA, Mike Mushi, amesema ukosefu wa mitaji ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili vijana wenye mawazo ya biashara, hasa wale wasiokuwa na dhamana zinazohitajika na taasisi za kifedha.

Amesema chama hicho kinashirikiana na Serikali kuboresha mazingira yatakayowawezesha wajasiriamali kupata fedha za kuendeleza bunifu zao.

“Tunashirikiana na Serikali kuhakikisha kunakuwa na nyenzo nzuri za kusaidia vijana ambao hawana dhamana waweze kupata mitaji ya kukuza mawazo yao,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema ubunifu ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ikiwamo kujenga uchumi wenye thamani ya Dola trilioni moja.

Amesema matumizi ya teknolojia katika kilimo, usafirishaji, masoko na biashara yanaweza kuongeza ufanisi, thamani ya bidhaa na fursa za ajira.

Londo amewataka vijana kutumia ushirikiano wa kimataifa kujifunza teknolojia na kuboresha ushindani wa biashara zao.

Amesema mawazo ya vijana na matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali yana nafasi muhimu katika kutatua changamoto za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa biashara.

“Bila shaka mawazo ya vijana na namna wanavyoweza kutumia teknolojia katika sekta mbalimbali yana nafasi chanya ya kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo,” amesema.

Source link

Leave a Reply