HESLB ilivyopunguza muda kutoa mikopo hadi siku mbili

HESLB ilivyopunguza muda kutoa mikopo hadi siku mbili

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepunguza muda wa utoaji fedha za mikopo kwa wanafunzi kutoka mwezi mmoja hadi siku mbili, huku ikipanga kuunganisha mifumo yake na ya taasisi nyingine za Serikali ili kuongeza kasi ya huduma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia, amesema maboresho ya mifumo ya kidijitali yameongeza ufanisi wa huduma na kurahisisha wanafunzi kuomba mikopo, kujithibitisha na kufuatilia akaunti zao kupitia simu janja.

Amesema bodi hiyo imeweka mkazo katika kuhakikisha mikopo inatolewa kwa uwazi na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, bila upendeleo au kutegemea kufahamiana na watu wenye mamlaka.

Kiwia ameyasema hayo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, wakati HESLB ilipopokea cheti cha kimataifa cha ISO 9001:2015, kinachoweka viwango vya usimamizi wa ubora katika taasisi na utoaji wa huduma.

Amesema HESLB imepitia mabadiliko makubwa kutoka mfumo wa zamani uliotegemea makaratasi na magari ya halmashauri kukusanya maombi hadi matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

“Tunataka kuunganisha mifumo ili fedha ziweze kutoka ndani ya muda mchache baada ya maombi kukamilika,” amesema.

Amesema bodi hiyo inaendelea kuboresha mifumo yake ili kuongeza kasi ya utoaji huduma, kuimarisha usalama wa taarifa za wanafunzi na kuhakikisha majukumu yake yanatekelezwa kwa weledi.

“Hatutaki kumuonea wala kumpendelea mtu, ndiyo sababu nawasisitiza watumishi wenzangu wa bodi tuendelee kufanya kazi kwa weledi, mifumo ifanye kazi kwa ufanisi na tutaendelea kuiboresha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Ashura Katunzi, amesema kupata cheti cha ISO 9001:2015 ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa ubora na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Amesema kiwango hicho cha kimataifa kinaziwezesha taasisi kuweka taratibu za kazi, kutathimini vihatarishi na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Kwa HESLB, amesema udhibitisho huo unaimarisha mifumo ya utoaji mikopo na kuongeza imani ya wadau kuhusu taratibu zinazotumika kubaini wanafunzi wanaostahili kunufaika.

“ISO 9001 ni kiwango mama kinachowezesha taasisi kusimamia ubora wa huduma na kuongeza tija katika utendaji kazi,” amesema.

Dk Katunzi ameishauri HESLB kuendelea kuboresha mifumo yake kwa kuzingatia viwango vingine vya kimataifa, ikiwamo ISO 27001 kinachohusu usimamizi wa usalama wa taarifa na ISO 37001 kinachohusu mifumo ya kupambana na rushwa.

Akijibu ushauri huo, Dk Kiwia amesema bodi imetenga bajeti ya kuanza mchakato wa kupata vyeti hivyo mwaka 2027, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa taarifa na mifumo ya kudhibiti rushwa.

Amesema wataalamu waliofanya tathmini ya usalama wa mifumo ya HESLB, ikiwamo majaribio ya kubaini udhaifu unaoweza kutumiwa kuingilia mifumo hiyo, walibaini kuwa mifumo ya data imepangwa vizuri na ina uimara.

Katika hatua nyingine, Dk Katunzi amezitaka taasisi za Serikali na sekta binafsi kuwekeza katika mifumo ya usimamizi wa ubora ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Source link