Mbeya. Wakati bajaji zikirejea kwa mafungu jijini Mbeya, baadhi ya magari binafsi yameanza kubeba abiria kutokana na uhaba wa daladala.
Hali hiyo imejitokeza ikiwa ni siku ya nne tangu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Jumanne Sagini, atoe agizo la kuondolewa kwa bajaji katika barabara kuu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuweka utaratibu wa usafiri jijini humo.
Hata hivyo, licha ya agizo hilo, baadhi ya bajaji zimeonekana zikiendelea na shughuli zake katika barabara kuu, huku nyingine zikishusha abiria katika stendi ya daladala ya Kabwe.
Baadhi ya gari binafsi zikibeba abilia stendi ya daladala Kabwe jijini Mbeya.
Asubuhi ya leo Alhamisi, Oktoba 22, Mwananchi imetembelea stendi za Kabwe na Soweto na kushuhudia baadhi ya magari binafsi pamoja na guta yakibeba abiria. Baadhi ya bajaji nazo ziliendelea na shughuli zake, zikiwemo kutumia barabara kuu.
Wakati huohuo, vyombo vya ulinzi na usalama vimeonekana katika maeneo hayo kuimarisha ulinzi na usalama, huku huduma za daladala zikionekana kuwa haba.
Pikipiki za biashara, maarufu bodaboda nazo zimekuwa miongoni mwa vyombo vinavyochukua fursa hiyo kwa kubeba abiria, huku baadhi ya waendeshaji wakipanga nauli zao kutokana na changamoto ya upatikanaji wa usafiri.
Gari la Polisi likiweka ulinzi na usalama stendi ya Kabwe
Adela Mwakisole amesema kutokana na changamoto ya usafiri, nauli zimepaa akiiomba serikali kuona namna ya kulegeza makali ili kuwapunguzia maumivu ya nauli.
“Nauli zimepanda sana, usafiri hakuna, tunalipa kati ya Sh 2000 hadi Sh 5000 kwa guta, Kiri kuu, changamoto ni kubwa, serikali ilitazame hili hatuna kipato,” amesema.
“Lakini waboreshe barabara kama ilivyo Makambako Bajaji zipite pembeni vinginevyo tutazalisha wapiga nondo mtaani, vijana waruhusiwe kufanya kazi,” amesema Adela.
Kwa upande wake Joel Samuel amesema wanapitia wakati mgumu ikizingatiwa hali ya biashara kwa sasa imekuwa ngumu kutokana na changamoto ya usafiri akiomba serikali kuingilia kati.
“Tutakufa na njaa, biashara zetu wengine ni ndogo, ukiangalia nauli ya kutoka Mbalizi kuja mjini au Uyole si mchezo, watu waruhusiwe kufanya kazi, hali ni ngumu mtaani,” amesema Samuel.



Leave a Reply