Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anatarajia kuanza mgomo wa kula na kuacha kutumia dawa anazotumia kutokana na matatizo yake ya kiafya kuanzia kesho akipinga kile chama hicho inadai kuwa ni ukiukaji wa amri ya Mahakama Kuu kuhusu haki yake ya kuzungumza na mawakili wake kwa faragha akiwa Gereza la Ukonga.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amesema maofisa wa Magereza wameendelea kusimamia mazungumzo ya Lissu na mawakili wake licha ya hukumu iliyotolewa Oktoba 16, 2026, katika shauri namba 7300, iliyoelekeza mazungumzo hayo yafanyike bila kusikilizwa na maofisa, ingawa wanaweza kuwaona kwa ajili ya usalama.
Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, Oktoba 24, 2026, Dk Nshala amesema mawakili wa Lissu walimtembelea gerezani Oktoba 17 na 18, lakini hawakuruhusiwa kuzungumza naye kwa faragha. Amesema hali hiyo ilijirudia Oktoba 23 alipokwenda mwenyewe kumtembelea.
Katika hukumu hiyo, jopo la majaji Amir Mruma, Angelo Rumisha na Evaristo Longopa lilielekeza maofisa wa Magereza kulinda usalama bila kusikiliza mazungumzo ya mahabusu na mawakili wao. Pia, nyaraka za kisheria ziliruhusiwa kukaguliwa bila kusomwa au kuchukuliwa.
Mwanasheria wa Chadema, Rugemeleza Nshala, akizungumza na wanahabari Makao makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam, Jumamosi Oktoba 24, 2026.
“Mahakama iliagiza kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa anayo haki ya kuonana na kuongea na wakili wake bila kusikilizwa na maofisa wa Magereza, bali kwa kuonekana tu, lakini Magereza inavunja amri hiyo waziwazi,” amesema Dk Nshala.
Amesema Oktoba 23 alifika Gereza la Ukonga saa 7 mchana, lakini aliingia saa 10 jioni. Alipofika, maofisa walimweleza kuwa Lissu amekataa kuonana naye kwa sababu mazungumzo yasingekuwa ya faragha.
Dk Nshala amesema alipinga utaratibu huo, lakini baada ya Lissu kuletwa, alikataa kuzungumza katika mazingira ambayo maofisa wangesikiliza mazungumzo yao.
“Lissu alisema kutokana na amri ya Mahakama, sitakubali kufanya maongezi haya yaliyo kinyume na amri ya Mahakama. Kama nipo mahakamani hapa kwa mujibu wa mahakama nikishiriki maongezi haya, maana yake na mimi nitakiuka amri ya Mahakama,” amesema Dk Nshala, akinukuu maneno ya Lissu.
Mkuu wa Magereza afuatilia malalamiko
Alipotafutwa na Mwananchi kuhusu malalamiko hayo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Jeremiah Katungu amesema anafuatilia suala hilo ili kubaini kilichotokea na kupata ufumbuzi.
“Taarifa hii ndiyo naipata kwako mwandishi. Ninachofahamu, suala hili lilikuwa mahakamani na lilishatolewa uamuzi. Nifuatilie kwa wenzetu huko ili tujue kilichotokea na pa kuanzia ili kulishughulikia,” amesema.
Chadema yataka haki za mahabusu zilindwe
Akizungumzia uamuzi wa Lissu kugoma kula, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesema hatua hiyo inatokana pia na kutokuwa na imani na chakula anachopewa gerezani kutokana na kile alichodai kuwa ni ukiukaji wa amri ya Mahakama.
“(Lissu) Alisema kwa namna Mahakama inavyovunja amri ya mahakama, hana imani na chakula anachopewa gerezani hapo, hivyo ameamua kugomea chakula,” amesema Mnyika.
Mnyika amesema Chadema ilituma mawakili na watu wengine kumtembelea Lissu na kumfikishia ujumbe wa shukrani, lakini hawakupata nafasi ya kufanya hivyo. Amesema hali hiyo inaleta wasiwasi kuhusu ulinzi wa haki za mwenyekiti huyo zinazolindwa kikatiba.
“Ninatoa wito kwa ndugu na wapigania haki wote kuungana na Lissu kwa vitendo, ikiwemo mgomo wa kula ili kutuma ujumbe wa kudai haki za mahabusu wote nchini kulindwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mnyika.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumza na wanahabari Makao makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam, Jumamosi Oktoba 24, 2026.
Ameongeza kuwa mwanachama wa Chadema, John Pambalu, aliyekamatwa na kufunguliwa mashtaka hivi karibuni, naye amewekewa utaratibu unaoruhusu kutembelewa na ndugu wa familia na mawakili waliotambuliwa pekee. Kwa mujibu wa Mnyika, hali hiyo inaendeleza tatizo la mahabusu kunyimwa haki zao za msingi.
“Kufuatia hatua hii, chama kinajiandaa kwa hatua zaidi baada ya kufanya tathmini na kujua hatua za kuchukua ili kulinda haki za mahabusu kukutana na mawakili na ndugu zao kwa mujibu wa sheria,” amesema Mnyika.



Leave a Reply