Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Tabora, imewaachia huru Hamisi Kusailwa, Kulwa Masanja na Mayunga Shija, waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kumuua Dase Kusailwa, baada ya kubaini mapungufu katika ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Miongoni mwa sababu zilizochangia uamuzi huo ni tofauti katika maelezo ya maungamo yaliyodaiwa kutolewa na washtakiwa, dosari katika mnyororo wa uhifadhi wa sampuli za DNA na alama za vidole, pamoja na mapungufu katika utaratibu wa gwaride la utambuzi.
Mauaji hayo yalidaiwa kutokea usiku wa Agosti 24, 2022, katika Kijiji cha Bujulu, Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, ambapo Dase anadaiwa kushambuliwa kwa mapanga akiwa amelala na ndugu zake nyumbani kwa baba yake.
Hukumu ya kuwaachia huru washtakiwa hao ilitolewa Oktoba 19, 2026, na Jaji Martha Mpaze, ambaye alisema ushahidi wa upande wa mashtaka haukuthibitisha kwa kiwango kinachotakiwa kisheria kuwa washtakiwa hao walihusika na kifo hicho.
Nakala ya hukumu hiyo iliwekwa kwenye mtandao wa Mahakama. Hamisi, mshtakiwa wa kwanza, alikuwa ndugu wa marehemu.
Ushahidi wa upande wa mashtaka
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 16 na vielelezo 17 ili kuthibitisha shtaka la mauaji dhidi ya washtakiwa hao chini ya vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, usiku wa Agosti 24, 2022, Dase alikuwa amelala katika nyumba ya baba yake pamoja na ndugu zake, watu wawili wasiojulikana walipodaiwa kuingia chumbani na kumshambulia kwa mapanga mara kadhaa.
Watu hao walidaiwa kukimbia baada ya kuhakikisha kuwa Dase amekufa.
Shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, ambaye ni daktari aliyeuchunguza mwili wa marehemu, alieleza kuwa alibaini majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili na kuhitimisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa kupoteza damu nyingi.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa baada ya Hamisi kukamatwa, alikiri kuhusika na mauaji hayo na kuwataja washtakiwa wenzake pamoja na mtu mwingine wa nne ambaye hakukamatwa.
Shahidi wa nne wa Jamhuri, ambaye ni Hakimu wa Amani, Mwanaidi Ntemi, alidai kuwa alichukua maelezo ya nje ya mahakama kutoka kwa washtakiwa wote watatu.
Aidha, mahakama ilisikia kuwa Kulwa na Mayunga waliwaongoza polisi hadi maeneo ya vichakani ambako mapanga mawili yaliyodaiwa kutumika katika mauaji hayo yalipatikana.
Sampuli za damu na alama za vidole zilichukuliwa kwenye mapanga hayo na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Pia, gwaride la utambuzi lilifanyika Septemba 3, 2022, ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa walitambuliwa.
Katika utetezi wao, washtakiwa wote watatu walikana kuhusika na mauaji hayo na kupinga ushahidi uliotolewa dhidi yao.
Hamisi alidai kuwa wakati mauaji hayo yakitokea alikuwa nyumbani kwake Songambele, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
Alikana kuwahusisha washtakiwa wenzake na tukio hilo, akidai kuwa polisi walimtesa na kumlazimisha kusaini nyaraka ambazo hakusomewa.
Kwa upande wake, Kulwa alidai kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake pamoja na familia yake. Alikana kuwafahamu washtakiwa wenzake na kupinga madai kuwa aliwaongoza polisi hadi eneo ambako mapanga yaliyodaiwa kutumika katika mauaji hayo yalipatikana.
Alidai pia kuwa polisi walimtishia na kumlazimisha kusaini nyaraka bila kujua kilichoandikwa ndani yake.
Mayunga naye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake pamoja na mkewe. Alikana kuhusika na mauaji hayo, akidai kuwa polisi walimtesa, kumlazimisha kushika panga na kusaini maelezo ambayo hakuyatoa.
Washtakiwa wote watatu pia walikana kushiriki gwaride la utambuzi lililofanyika Septemba 3, 2022.
Katika uchambuzi wa ushahidi, Jaji Mpaze amesema ingawa upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa Dase aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye makali, haukuthibitisha bila kuacha shaka yenye msingi kuwa washtakiwa hao ndio waliohusika na tukio hilo.
Miongoni mwa mapungufu aliyoyabainisha ni tofauti katika maelezo yaliyodaiwa kuwa maungamo ya washtakiwa, hususan jina la mtu aliyedaiwa kuuawa.
Jaji amesema katika maelezo ya Hamisi, jina lililotajwa lilikuwa Ngasa Kusailiwa, wakati katika hati ya mashtaka marehemu alitajwa kuwa Dase Kusailwa.
Mahakama ilieleza kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa majina hayo mawili yalikuwa yakimrejelea mtu mmoja.
Pia, Jaji Mpaze amesema ushahidi kuhusu mapanga yaliyodaiwa kutumika katika mauaji hayo haukuwasilishwa kwa namna iliyoondoa mashaka kuhusu uhusiano wake na tukio hilo.
Amesema kulikuwa na mapungufu katika maelezo ya namna sampuli za damu na alama za vidole zilivyokusanywa, kuhifadhiwa na kuwasilishwa kwa wataalamu kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa mahakama, dosari hizo zilifanya ishindwe kuwa na uhakika kuwa sampuli zilizochunguzwa na wataalamu zilikuwa zilezile zilizokusanywa katika eneo la tukio.
Katika suala la gwaride la utambuzi, Jaji amesema kulikuwa na mapungufu, yakiwemo kutokuwepo kwa maelezo ya kutosha kuhusu namna washtakiwa walivyoelezwa haki zao kabla ya hatua nyingine kuendelea.
Kutokana na hali hiyo, mahakama iliona kuwa ushahidi wa gwaride hilo hauwezi kutegemewa peke yake kuthibitisha utambulisho wa wahusika.
Mahakama yaeleza msingi wa kuwaachia huru
Jaji Mpaze amesema katika kesi za mauaji, upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yenye msingi, huku akisisitiza kuwa udhaifu wa utetezi wa mshtakiwa hauwezi kutumika kuziba mapungufu katika ushahidi wa mashtaka.
“Kushindwa kwa washtakiwa kutoa utetezi unaoridhisha hakuwezi kurekebisha mapungufu yaliyopo katika kesi ya upande wa mashtaka,” amesema Jaji Mpaze.
Ameeleza kuwa ushahidi wa mazingira unaotumika kuthibitisha kosa unapaswa kuunda mnyororo kamili wa ushahidi unaowaunganisha washtakiwa na tukio, huku ukiondoa uwezekano mwingine unaoweza kueleza kilichotokea.
“Katika kesi hii, mahakama iliona kuwa ushahidi uliowasilishwa haukufikia kiwango hicho. Kutokana na sababu hizo, mahakama inahitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kuwa washtakiwa hawa walisababisha kifo cha Dase,” amesema.
Kwa msingi huo, mahakama imewakuta Hamisi, Kulwa na Mayunga hawana hatia ya mauaji na kuamuru waachiwe huru mara moja, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.


