Kamani: Wilaya zote ziige mfano wa Mufindi

Kamani: Wilaya zote ziige mfano wa Mufindi

Mufindi. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amezitaka wilaya zote nchini kuiga mfano wa Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, kwa kuandaa na kuboresha maonyesho ya biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuvutia wawekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi.

Kamani ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, wakati akifunga Maonyesho ya Biashara na Uwekezaji ya Mufindi, yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Wambi, ndani ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga.

Amesema halmashauri na wilaya zote nchini zinapaswa kuanzisha maonyesho ya aina hiyo, akieleza kuwa Mufindi imeonyesha kwa vitendo namna ya kutafsiri Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa kuibua na kutumia fursa zilizopo katika eneo husika.

“Kwa namna ya kipekee, nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, kupitia uongozi wake kwa kuonyesha kwa vitendo namna ya kutafsiri Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa kuzingatia fursa, mahitaji na mazingira halisi ya wilaya hii,” amesema Kamani.

Amesema kuandaa maonyesho hayo kwa mara ya kwanza ni hatua muhimu inayoonyesha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo si nyaraka ya kusoma pekee, bali ni mwongozo wa kuchochea ubunifu, kuvutia wawekezaji, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

“Sisi kama Serikali, wizara zote tuna wajibu wa kuwaunga mkono. Nawaahidi tutawaunga mkono katika uwekezaji wowote mtakaoufanya katika Wilaya ya Mufindi,” amesema.

Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi Ng’wasi Kamani akisiliza maelezo yaliyolewa na Msimamizi wa wakala wa mbegu Tanzania (ASA) Mkoani Iringa Vaison Mwaluseke alipotembelea banda hilo katika maonyesho ya biashara na uwekezaji Mufindi Investment Forum and Expo 2026 katika viwanja vya shule ya msingi wambi.

Katika hatua nyingine, Kamani amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo thabiti itakayohakikisha juhudi za kuendeleza biashara na uwekezaji zinaendelea hata baada ya maonyesho hayo, ili wananchi wa Mufindi waendelee kunufaika.

Amesema misingi inayowekwa kupitia maonyesho hayo inaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga sekta binafsi kuwa na mchango wa asilimia 70 katika uchumi wa nchi.

“Misingi tunayojenga hapa ni muhimu, kama dira yetu ya maendeleo inavyosema kuwa asilimia 70 ya uchumi wetu utashikiliwa na sekta binafsi. Hivyo, maonyesho haya ni muhimu sana katika kutekeleza dira hiyo,” amesema.

Dk Salekwa amesema tangu maonyesho hayo yalipozinduliwa Oktoba 16, yamehudhuriwa na wananchi zaidi ya 40,000 waliopata fursa ya kujifunza na kutambua fursa mbalimbali katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema maonyesho hayo yamekuwa fursa kwa vijana kukutana na wawekezaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuwasaidia kukuza ubunifu wao, kupata masoko na kuongeza kipato.

Salekwa amesema jukwaa la uwekezaji lililoandaliwa katika maonyesho hayo pia lililenga kuwahamasisha wananchi kujiajiri kwa kutumia fursa mbalimbali zilizotolewa kupitia mijadala hiyo.

Mratibu wa maonyesho hayo,  Bonifance Mligo amesema maonyesho hayo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Wilaya ya Mufindi kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inatekelezwa kwa vitendo.

“Jitihada hizi zinalenga kuhamasisha uwekezaji, kukuza uchumi na kuongeza ajira, sambamba na kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Mligo.

Awali, Msimamizi wa Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) Mkoa wa Iringa, Vaison Mwaluseke alisema wakala huo umetumia maonyesho hayo kuwafikia wakulima na kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora, hasa wakati huu wa kuelekea msimu wa mvua.

Amesema ASA ilishiriki maonyesho hayo ikiwa na mbegu mbalimbali za mazao ya kilimo, zikiwemo alizeti, maharage, mahindi, mpunga na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mbegu hizo.

Source link